SERIKALI wilayani Kilosa Mkoa wa Morogoro, imesema wakati huu ambapo dunia inakabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, ipo haja dhana ya utunzaji shirikishi wa vyanzo vya maji ikapewa kipaumbele ili kuokoa rasilimali hiyo muhimu kwa maisha ya binadamu.

Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Kilosa, Cheyo Nkelege wakati wa uzinduzi wa Ofisi ya Jumuiya ya Watumia Maji katika Kijiji cha TAMI / MSOWERO, ambapo ujenzi wake umesimamiwa na Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu.

Aidha, sambamba na mabadiliko ya tabianchi yanayotajwa kuhatarisha uhai wa rasilimali maji, changamoto nyingine inayotajwa ni ongezeko la shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo hivyo, zinazosababisha hali ya uchafuzi wa mazingira.

Kwa upande wake mwakilishi kutoka Wizara ya Maji, Norah Hambya ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvi, alisema dhamira ya ujenzi wa ofisi ya Jumuiya ya watumaji maji katika eneo hilo utasidia ulinzi na uhifadhi endelevu wa rasilimali maji.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Msowero, wameelezea namna Jumuiya za Watumia maji zinavyosaidia kutunza na kulinda vyanzo vya maji katika eneo hilo.

Katika hatua nyingine, imeelezwa kuwa mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Jumuiya ya Watumia Maji Katika Bonde Dogo la TAMI / MSOWERO wilayani Kilosa hadi kukamilika umegharimu kiasi cha Shilingi Milioni 72.