BODI ya Maji Bonde la Wami/Ruvu imetangaza zabuni ya kumpata mshauri elekezi atakayefanya utafiti jinsi ya kuvuna maji ya mvua ili kuyahifadhi katika chanzo cha maji cha Mzakwe Makutupora ambacho ni chanzo pekee cha maji kwa wakazi wa Dodoma ili kwendana na ongezeko la watu katika jiji hilo.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Bodi ya Maji wa Bonde hilo, Simon Ngonyani wakati akizungumza na Nipashe baada ya bodi hiyo kutembelea chanzo hicho kwa lengo la kujionea changamoto zilizopo na kuzipatia majibu kwa ajili ya kuhakikisha zinatatuliwa.

Ngonyani alisema shughuli za Serikali zote zimehamia Dodoma ambapo ni makao mkuu ya nchi na wakazi wake wanategemea maji kutoka chini ya ardhi ambapo chanzo cha Mzakwe Makutupola ndio chanzo pekee cha maji kinachotengemewa huku matumizi ya maji yakiongezeka.

“Kwa sasa kuna zabuni ambayo tumetangaza ya kumpata mshauri elekezi afanye utafiti jinsi ya kuvuna maji ya mvua na sisi tuyatibu ili baadae tuyaelekeze katika bonde hili yaingie chini, yaani kama benki ya maji kwa ajili ya matumizi ya baadae na hii ni inakuwa tahadhari ili chanzo hichi kiwe na maji ya kutosha,” alisema Ngonyani

Aliongeza kuwa Bonde la Wami/Ruvu wanajukumu kubwa la kuhakikisha wanahifadhi chanzo cha Mzakwe ili kiweze kufikia uhitaji wa kutosheleza mahitaji ya wakazi wa Dodoma wakati Wizara ya Maji wakitafuta chanzo kingine cha maji.