Serikali imepiga marufuku uchimbaji mchanga, kilimo na ujenzi wa makazi katika vyanzo vya maji ili kukabiliana na uharibifu wa kingo za mito na kusababisha mafuriko ya mara kwa mara Tegeta, Bunju na maeneo mengine ya mkoa wa Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Maji Bonde la Wami Ruvu Simon Ngonyani ameyasema hayo wakati yeye na viongozi wengine walipotembelea Bonde la Mto Tegeta ambako baadhi ya nyumba za wananchi zinasombwa na maji kipindi hiki cha mvua.

Katika ziara hiyo Ngonyani ameshuhudia shughuli za kibinadamu kando ya bonde hilo zikiwa zinaendelea. Amesema wakati umefika sasa kwa wananchi kuacha tabia ya kujenga nyumba kwenye mito na mabondeni, kwani kuna uwezekano mkubwa wa maji kuama na kuharibu makazi ya watu.

"Tunaomba wananchi mtusaidie muache kukaa kwenye mabonde na mito, mkiona eneo la bonde msiweke makazi kwani hiyo itasaidia nyumba kutoondoka na maji,” amesema.