Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso amezindua Mradi wa Huduma ya Maji na Birika la Kunyweshea Mifugo Katika Kijiji cha Ruvu Darajani Uliogharimu Kiasi cha Shilingi Millioni 65 ambao utanufaisha Zaidi ya Mifugo 2000 kunywa maji kwa siku pamoja na kutoa huduma ya maji safi kwa wakazi wa vijiji jirani vinavozungukwa na Mradi.

Mradi huu umetekelezwa na Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu kwa kushirikiana na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za kusini mwa Afrika (SADC), chini ya mpango wa GCCA+ Intra-ACP (Global Climate Change Alliance) wenye lengo la kuweka usimamizi mzuri wa Rasilimali za maji, uhifadhi wa mazingira na kuzuia mmomonyoko wa udongo na uchafuzi wa vyanzo vya maji unaosababishwa na mifugo. 

Waziri Aweso ameipongeza Bodi ya maji Bonde la Wami/Ruvu na Taasisi ya Global Water Parternship(GWP) kwa utekelezaji Mzuri wa Mradi huu na kuitaka Mamlaka ya Usambazaji wa maji na Usafi wa Mazingira Vijijini RUWASA mkoa Pwani kusimamia kwa umakini mradi huu pamoja na kubuni Miradi mingine itakayosaidia wafugaji wa Halmashauri ya Bagamoyo. 

Pia kwa upande wa Naibu katibu mkuu Wizara ya Maji Mhe. Cyprian Luhemeja ameishukuru Bodi ya maji Bonde la Wami/Ruvu pamoja na Taasisi ya GWP kwa kuleta mradi huu wilayani Bagamoyo ambao utasaidia sana katika kipindi cha ukame. Naye Mbunge wa chalinze Mheshimiwa Ridhwani Kikwete ameyataka mabonde mengine kuiga Mfano wa Bonde la Wami/ Ruvu katika utekelezaji wa shughuli zake. Vilevile mradi huu utapunguza shida ya maji na usumbufu wa mifugo katika vyanzo vya maji. 

Aidha Mwenyekiti wa Bodi ya maji Bonde la Wami/Ruvu Bi Hafsa  Mtasiwa amewataka wananchi wa wilaya ya Chalinze kutoa ushirikiano katika utunzaji  na maendeleo ya mradi huu huku  Mwenyekiti wa wafugaji mkoa wa Pwani ameshukuru kwa Wizara ya Maji kupitia kwa Waziri Aweso kuwa birika hili la mfano ni ukombozi kwa maisha ya Wafugaji na kupunguza athari za uvamizi katika vyanzo vya maji kwani mifugo itakuwa imeupuka kwenda mtoni na kusaidia kuepuka kushambuliwa na wanyama wakali.