Uhaba wa maji huenda ukaikumba miji ya Dar es Salaam na Pwani katika kipindi cha miezi miwili ijayo, ambapo kujitokeza kwa changamoto hiyo ni baada ya kupungua kwa kina cha maji katika mto Ruvu ambao unasambaza maji kwa Wananchi wa mikoa hiyo miwili.

Shughuli mbalimbali za Kibinadamu pamoja kiwango kidogo cha mvua ni miongoni mwa Sababu zinazotajwa kupelekea kupungua kwa kina hicho cha maji katika mto Ruvu.

Kaimu Mkurugenzi Bodi ya maji bonde la Wami Ruvu Elibariki Mmasi, akizunguma mara baada ya kufika na kukagua chanzo cha maji mto Ruvu, amesema kina cha maji kimezidi kupungua tofauti na ilivyokuwa Septemba mwaka jana.

Mmasi ameongeza kuwa Shughuli za Kibinadamu pamoja na kutokuwepo kwa mvua za Kutosha ni Sababu ambazo zinachangia pakubwa kutokea kwa hali hiyo.

Kufuatia hali hiyo Kaimu mkurugenzi huyo wa Bodi ya maji Wami Ruvu ametoa rai kwa Wananchi hususani wa Dar es Salaam na Pwani kutumia maji kwa uangalifu ili kukabiliana Changamoto hiyo.

Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu ni Taasisi ya Serikali inayoshughulika na uhifadhi, utunzaji na uendelezaji wa vyanzo vya maji hapa nchini.